Akizungumza kwa hisia kali, kijijini kwake Ibula, katika kata ya Kiwira, wilayani Rungwe, Mama mzazi wa Marehemu, Esther Mwambenja, alisema kabla ya tukio hilo kutokea kulikuwa na viashiria vingi vya mumewe kufanya ukatili.
Alisema tukio la mzazi mwenza huyo kumwiba mtoto na kwenda kumfanyia ukatili huo wa kinyama lilikuwa la pili, baada ya awali kumuiba akiwa na miaka miwili na miezi mine na alimrudisha kwa maandishi ya serikali ya kijiji.
Alisema katika tukio la kwanza la mtalaka wake huyo kumuiba mtoto wao huyo, lilitokea Septemba mwaka 2012, baada ya wiki chache za kumfukuza katika nyumba waliyokuwa wakiishi katika kitongoji cha Iponjola, kijiji cha Asenga, nyumba iliyotumika kuzikwa mtoto huyo.
MAITI YA DEBORA |
Alitaja sababu za yeye kufukuzwa ni ugomvi uliotokana na yeye kuhoji sababu za kuficha fedha kiasi cha sh. 120,000 zilizotokana na wao kwa pamoja kufanya kazi ya kibarua katika mashamba kijijini hapo na baada ya malipo kutolewa mtalaka wake huyo alionesha kiasi kidogo cha sh.80,000.
Alisema ugomvi huo ndio ulisababisha yeye arudishwe kwa wazazi wake, lakini baada ya muda mfupi mwanaume huyo alimfuata na kumbembeleza ili warudiane na alipogoma aling’ang’ania aondoke na mtoto .
“Nakumbuka ilikuwa Novemba mwaka jana baada ya mimi kuondoka nyumbani kwake na kurudi kuishi hapa nyumbani, siku hiyo tukiwa shambani huyo bwana alikuja hapa nyumbani na kumkuta mwanangu wa kwanza (Neema Steven ) niliyezaa na mwanaume mwingine” alisema Mwambenja.
Alisema baada ya kufika eneo hilo majira ya saa mbili asubuhi alitumia ujanja na kufanikiwa kumuiba mtoto na kisha kutokomea naye kijijini kwao Asenga, hali ambayo ilisababisha kutoa taarifa kituo cha polisi Kiwira.
“Unajua kuwa baada ya kwenda kutoa taarifa polisi walitusaidia kufika kijijini kwao ambapo serikali ya kijiji ilikubali nimchukue mwanangu kwa kuwekeana mkataba wa kisheria kwa mujibu wa sheria, kwani alikuwa chini ya miaka saba”.
Aliongeza kuwa Novemba 15 mwaka 2012 serikali ya kijiji chini ya Mwenyekiti, Lutengano Mwakyoma na mashahidi watano wakiwemo wazazi na ndugu zake, walinikabidhi barua ya kuridhia kuondoka na mwanangu, huku ikimuonya mume wangu kutorudia kosa hili la kumuiba mtoto hadi hapo atakafikisha miaka saba.
MTOTO DEBORA ENZI ZA UHAI WAKE |
Tukio la pili la kuiba mtoto.
Alisema tukio hilo lilitokea Novemba 29 mwaka jana 2012, ambapo alifika nyumbani kwao majira ya saa 12 :00 na kumkuta dada wa marehemu kumchukua mtoto akimdanga kuwa anaenda kusenya kuni eneo la jirani.
Aliongeza kuwa baada ya kuona dada wa marehemu anang’ang’ania kwenda wote alimuamuru arudi nyumbani kuchochea moto kwa kuwa kulikuwa kumeinjikwa mboga na kukubali kurudi.
“kwa mujibu wa maelezo ya mwanangu huyu wa kwanza alisema baada kurudi toka ndani, alikuta baba yake huyo ameondoka na mtoto na tuliporudi na kupokea taarifa hizo tulichanganyikiwa na kuanza kuhangaika hovyo” alisema mama wa marehemu.
Mwambenja alisema kuwa baada ya kucha siku ya pili asubuhi yake
walienda kutoa taarifa kituo cha polisi cha Kiwira ili waweze kupata msaada wa kumtafuta, huku wakionesha barua ya makubaliano ya awali ya yeye kuwa na haki ya kisheria ya kusimamia malezi ya mwanao hadi afikishe miaka saba.
Alisema baada ya kutoa taarifa hizo kituoni hapo, askari aliyekuwa zamu siku hiyo alimtaka kutoa kiasi cha shilingi 50,000 ili fedha hizo wapewe askari mgambo wa kwenda kijijini kwa mzazi mwenzake huyo, kwani tayari walikuwa na taarifa kuwa alikuwa amekimbilia huko.
“Kutokana na hali ngumu ya maisha tulikosa kiasi hicho cha fedha hivyo suala hilo kubaki bila msaada wa polisi na pia hatukuweza kwenda kwa kijijini kwao”.
Aliongeza “sababu ya mimi kuwa mzito kuendelea kumfuatilia kijijini kwao kwa mara ya pili ili kujua kama yupo huko na mtoto ilitokana na hofu niliyoijenga, kwani awali tukiwa kwenye ugomvi alitamka maneno ya vitisho kuwa endapo nitaendelea kung’ang’ania kumchukua mtoto pale anapomchukua atakuja kumuua ili tukose wote”.
Hata hivyo mama huyo mzazi wa Debora, alisema kuwa baada ya kuona hali hiyo, aliendelea kuwasiliana na wifi yake , Bupe Mwangoka,ambaye ni dada mkubwa wa mume wake anayeishi eneo la Isanga Jijini mbeya, ambaye ndiye alisaidia kwa kiasi kikubwa kubainika kwa unyama aliofanya.
Maisha kabla ya tukio.
Akielezea maisha yao kabla ya kutengana na baadae kuamua kufanya ukatili huo, alisema aliwahi kumtamkia maneno makali wakati akiwa na ujauzito wa miezi nane .
Alisema baada ya kuibuka ugomvi katika kipindi hicho, mwanaume huyo alimtaka kwenda kuiuza mimba ile kwa mwanaume mwingine yeyote atakayempenda ili asije akazaa mtoto ambaye atachanganya damu ya koo hizo mbili.
“Maneno yale katika kipindi hicho sikuyatilia maanani kwani nilifikiri zilikuwa ni hasira, lakini leo hii ndio najua maana ya ile kauli ” alisisitiza Mwambenja.
Hata hivyo alisema inashangaza kwani kuna wakati tukiwa katika maisha ya kawaida kabla ya yeye kufanya tukio hilo, mara kadhaa alijutia na kuonya juu ya matukio machafu yaliyojitokeza na kusikika ya watu kuuawa au kuondolewa baadhi ya viungo vya miili yao.
Aidha, alieleza mkasa mwingine wa mume wake huyo ni ule wa wao kufukuzwa katika mji wa Kiwira walikokuwa wakiishi awali kwa kufanya shughuli za umachinga.
Alisema walitimuliwa na serikali ya mtaa katika mji huo kutokana na mumewe huyo kutuhumiwa kuiba simu ya mkononi ambapo alipokea kipigo kikali na baadae kufukuzwa.
Kutokana na hali hiyo, mama wa marehemu Debora alisema yote yaliyotokea amemwachia mungu na kwamba kama ingekuwa uwezo wake angeamuru naye anyongwe, hivyo mamlaka husika zitajua cha kufanya.
Kwa upande wake dada wa marehemu Debora, Neema Stevini(5) ambaye ni mtoto wa kufikia wa baba mzazi wa marehemu, akisimulia jinsi mdogo wake alivyoibwa , alisema kuwa anakumbaka mara ya mwisho ilikuwa jioni majira ya saa 12 jioni.
“Nilitaka kwenda nao, lakini baba Debora akaniambia nirudi kuchochea moto ndani na niliporudi nikakuta wameondoka na nilipokimbilia sana siku waona” alisema kwa masikitiko Neema.
Hata hivyo uchunguzi wa Mbeya yetu umebaini kuwa marehemu Debora alifariki dunia siku hiyo ya Novemba 29 mwaka jana, majira ya saa nne usiku baada ya baba yake kufanikiwa kumuiba kutoka nyumbani kwa mama yake.
Inadaiwa kuwa baada ya kufanikiwa kumtorosha baba huyo wa marehemu alitembea kwa mguu umbali wa kilomita 50 kutoka kijiji cha Ibula alikomuiba hadi nyumbani kwake kijiji cha Isange katika kata ya Isange.
Imeelezwa kuwa baada ya kufika nyumbani kwake, baba huyo mzazi wa marehemu alichimba shimo katikati ya sebule na kumchukua mtoto wake huyo akiwa usingizini na kisha kumfukia akiwa hai.
“Mwanaume Yule alikuwa katili sana, kwani baada ya kumfukia alichukua meza ya chakula na kuiweka juu yake huku akiipamba kwa magazeti jambo ambalo lilifanya ndugu zake wasigundue kirahisi” alisema mpasha habari.
Chanzo hicho kilisema baada ya kufanya hivyo aliishi kwa wiki moja na baadae kukimbilia Jijini Mbeya ili watu wasibaini juu kitendo alichofanya na kwamba kila alipohojiwa na ndugu zake alisema mwanae huyo alimuweka kwa rafiki yake Jijini Mbeya.
Hata hivyo baada ya danadana za muda mrefu ndipo dada wa mtuhumiwa huyo aliamua kutoa taarifa jeshi la polisi na kufanikiwa kumkamata akiwa katika harakati za kutorokea wilayani Chunya na alipobanwa alifichua siri ya alipo mwanae kwa kueleza kuwa alimuua na kumfukia ndani kwake.