Habari kubwa ni kwamba; Rostam Aziz kaachia ngazi CCM.Wengine wanasema, kuwa Rostam amejivua gamba. Kuna wanaodai, kuwa ni CCM ndio iliyojivua gamba. Ni misamiati tu, isikuumize kichwa.
Nimesoma hotuba ya Rostam akiongea na ’ Wazee wa Igunga’. Imekuwa utamaduni, kama wa enzizile za Mwalimu. Kwenye jambo zito, Mwalimu aliongea na ’ Wazee wa Dar es Salaam’. Sio ndio waliomkaribisha mjini.
Kuna akina sisi tulio tofauti na wale wanaodhani wanajua. Sie tunajitahidi kujua. Na hapa ni tafsiri yangu ya kuachia ngazi kwa Rostam Aziz. Kwangu mie ilikuwa ni suala la wakati tu; kuwa Rostam hakuwa na njia ya kutokea zaidi ya kukubali ’ kujiporomosha’ mwenyewe kutoka kwenye ngazi. Ndio, ni heri anayeshuka kwenye ngazi kuliko anayeachia ngazi na kuporomoka. Kushuka kwenye ngazi kunaashiria taratibu. Kuna upepo mgumu unavuma ndani ya CCM. Na upepo mwingine huangusha miti mikubwa.
Na Rostam huyu alikuwa ni sehemu ya ’ mapacha watatu’ kama wanavyojulikana sasa; Rostam , Andrew na Edward. Kuna wanaoanza kuhesabu siku kabla kusikia habari nyingine kubwa; kuwa Edward naye ’ kajiporomosha’ kutoka kwenye ngazi za CCM, kisha afutie Andrew. Yote hayo yanawezekana, lakini, kila inapoisha arobasitini moja , karata huchangwa upya. Hapo huanza arobasiti mpya. Siasa yaweza kuwa kama mchezo wa arobasitini! Na mazingira ya Rostam wa Unyamwezini Igunga yaweza kuwa tofauti na ya Andrew wa Usukumani na Edward wa Umasaini. Burudani ya siasa inaendelea!
Na Watanzania tu mabingwa wa siasa za matukio. Leo ni Rostam. Baada ya wiki moja Rostam si habari tena. Tunasubiri nyingine, labda itakuja ya Edward na baadae Andrew. Na ’ mapacha watatu’ wakishamalizika? Stay tuned; Kuna mpya nyingine itakuja.
Na Rostam pale Igunga kwa wazee wake amezungumzia ’ Afya ya siasa’ ya nchi. Hakusema kama ni njema au la. Katikati ya mistari kuna tulioelewa alichotaka kusema Rostam. Tena Rostam huyu ambaye kuna wakati iliaminika ndiye yuko nyuma ya ’ mikakati’ ya ndani ya Chama chake.
Leo kaacha kila wadhifa ndani ya Chama. Lakini usisahau, kuwa Rostam amebaki na ’ hirizi’ mfukoni. Ni kadi ya chama. Mjinga ni yule anayemwondoa Rostam mwenye ’ hirizi’ ya Chama kwenye ’ hesabu’ za mikakati ya CCM.
Na si amesema mwenyewe; kuwa haikuwa kazi rahisi kwao kuifanya Tabora ambayo ni kitovu cha upinzani kuwa mkoa ambao majimbo yote yanayoongozwa na CCM. Je, Rostam ’ anatishia nyau’ au kuna mtaji anawekeza kwenye ’ nyumba ’ya mchezo wa bao? Na tusubiri tuone.
Na hii afya ya siasa anayoizungumzia Rostam? Sijui yeye katumia vipimo vya kliniki gani. Mie nitapiga mbizi na kuzama zaidi majini. Na hapa unisome kwa makini . Ndio, kama nchi Watanzania ni kama wagonjwa tunaotafuta tiba. Na tumekuwa ni watu wa kubahatisha tiba kila kukicha. Hata kukimbilia abrakadabra ya kikombe cha ’ Babu wa Lolilondo’ ni kielelezo cha maradhi yetu na kuhangaika kwetu.
Mgonjwa hukosa faraja na huzidi kuwa na mashaka pale daktari anaposhindwa kufanya diagnos ya ugonjwa husika na kujua ni nini hasa chanzo cha maradhi. Kisha daktari anajaribu kumpa mgonjwa dawa akitumaini tu kuwa huenda ikamsadia. Lakini, mgonjwa hupata faraja na huingiwa matumaini ya kupona pale anapofanyiwa diagnos na daktari anapomtamkia mgonjwa chanzo cha maradhi ya kinachomsibu na dawa anayotakiwa kutumia ili apone.Na ndio sisi Watanzania; tu wagonjwa tunaofanyiwa majaribio ya dawa ya kutuponesha maradhi yetu bila haswa daktari kujua chanzo cha maradhi yetu.
Watanzania tunapaswa sasa kuvunja ukimya na kuzungumzia mema na mabaya yaliyopita ili yatusaidie kujenga misingi imara ya taifa letu hata kwa miaka 50 ijayo. Tuna wajibu wa kizalendo wa kutoa ushahidi wetu kwa kusimulia tuliyoyapitia ili waliopo na wajao waweze kuyachukua mema na kutorudia makosa yaliyofanyika nyuma.
Maana, kuna tulioshuhudia Tanzania iliyokuwa na ustawi na dalili za kuendelea kustawi. Tumeshuhudia pia ni kwa jinsi gani wingu hilo la matumaini lilivyokuwa likipotea kwa kasi ya kutisha na kupisha jua kali lililoleta ukame wa kisiasa na kiuchumi katika nchi yetu.
Na msingi wa haya yote ni ubaguzi wa kisiasa na kutoruhusu mazingira ya uwepo wa fikra mbadala. Kuwachukia wenye ’ akili’ na walio tayari kuzitumia akili zao kwa manufaa ya nchi yao. Hivyo basi, watu hao hutengwa na mfumo wa uongozi wa kisiasa uliopo.
Na huo ndio msingi wa uwepo w a hoja ya ubaguzi wa kisiasa. Na dhambi hii ya ubaguzi wa kisiasa ndilo gamba gumu la kitaifa tunalopaswa kulivua. Maana, ndio hali yenye kusababisha maradhi yetu mengi kama taifa ikiwamo ufisadi uliotamalaki.